Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewataka wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi wajiepushe na vitendo vya rushwa ili kuhakikisha miradi inayotekelezwa inalingana na thamani ya fedha inayotumika.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo jana wakati akifungua semina endelevu ya 29 ya Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi, iliyofanyika Jijini Dodoma.
’’Epukeni vitendo vya rushwa ambavyo huisababishia Serikali hasara kubwa na kuleta usumbufu kwa wananchi. Ni matumaini yangu kuwa mtafanya kazi kwa weledi na kufuata maadili ya taaluma zenu’’ Majaliwa.
Alisema wataalamu hao ni vema wakahakikisha majengo wanayobuni yanakuwa bora katika muonekano na mandhari yake iwe yenye kuvutia na yenye kuzingatia utunzaji wa mazingira na matumizi bora na endelevu ya nishati.
Aidha Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuipongeza Bodi ya Usajili wa Wabunifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi kwa kuchagua mada inayohusu jukumu la wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi katika kuendeleza viwanda hapa nchini.
Alisema anatambua kuwa ujenzi wa viwanda unaendana na ujenzi wa miundombinu kama majengo, barabara, madaraja, miundombinu ya nishati na viwanja vya ndege, ambayo ni muhimu katika kuimarisha uchumi wa viwanda.
"Hivyo, wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi mna mchango mkubwa sana katika kufikia uchumi wa viwanda. Nitoe rai kwa Bodi ihakikishe kuwa miradi yote ya majengo pamoja na miundombinu mingine inashirikisha wabunifu majengo na wakadiriaji majenzi katika ubunifu na usimamizi wa ujenzi wake.’’
No comments:
Post a Comment