WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali ya awamu ya tano itaendelea
kusimamia maadili ya utumishi wa umma ili kuenzi fikra za hayati Edward Moringe
Sokoine.
“Tutaendelea kusimamia maadili ya utumishi wa umma kwa kuzingatia yale
yote ambayo Mheshimiwa Sokoine aliyaanzisha,” amesema.
Ametoa kauli hiyo leo mchana (Alhamisi, Aprili 12, 2018) wakati
akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi waliohudhuria ibada ya kumbukumbu
ya miaka 34 ya kifo cha Sokoine, iliyofanyika kijijini kwake Engwiki, kata ya
Monduli Juu, wilayani Monduli, mkoani Arusha.
Ibada hiyo iliyoongozwa na Askofu Mkuu Mstaafu wa Jimbo Kuu
Katoliki la Arusha, Mhashamu Josephat Lebulu, ilihudhuriwa na viongozi wa
dini wa wilaya, viongozi wa Serikali na wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Waziri wa
Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi, Naibu Waziri wa Elimu,
Sayansi na Teknolojia, William Tate ole Nasha na baadhi ya wabunge.
Waziri Mkuu amesema Mhe. Sokoine alikuwa adui wa wahujumu uchumi na
alihakikisha uchumi wa nchi unakua kwa maslahi ya Watanzania wote. “Mungu
alitupa hazina iliyong'ara na kuangaza. Sote tuendelee kuangaza kwa kutenda
mema na kuendeleza yale yote aliyoyaanzisha mpendwa wetu,” alisema.
“Katika maisha yake, hakuwa na ubinafsi, uroho, wala tamaa ya
kujilimbikizia mali. Hili ni jambo la kuigwa na sisi viongozi wa umma. Nasi
tulioko kwenye nafasi hizi za uongozi, tumuombe Mungu atuwezeshe tutende
yale aliyoyaanzisha,” alisisitiza.
Alitumia fursa hiyo kuwafikishia wanafamilia na wananchi waliohudhuria
ibada hiyo, salaam za pole kutoka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,
Dkt. John Pombe Magufuli na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan.
Mapema, akizungumza na mamia ya wananchi waliohudhuria ibada hiyo, Askofu
Mst. Lebulu alimuelezea hayati Sokoine kuwa ni kiongozi aliyechapa kazi kwa
bidii, mwenye uzalendo, aliyeongozwa na upendo na uwajibikaji kwa wananchi
anaowaongoza.
“Ili tuweze kuwajibika na kuwa wazalendo kwelikweli, tunapaswa kuwa
waaminifu na watu tunaomcha Mungu. Mtu awaye wa dini yoyote ile, kama hamchi
Mungu, hawezi kuwa muwajibikaji.”
Alisema kila mtu anapaswa kumheshimu mwenzake kwa dini na imani yake.
“Tuheshimiane kila mmoja kwa dini na imani yake, kwa sababu sote tumeumbwa kwa
sura na mfano wake. Siyo kwamba tuvumiliane, tunatakiwa tusidharauliane bali
tuheshimiane,” alisisitiza.
“Ni lazima tuwe waaminifu, tuache unafiki, tuache kuwa na maisha yenye
hila na hiyana na badala yake, tuongozwe na dhamiri safi. Tuwe waaminifu kwa
wenzetu, kwa dini na imani zetu na zaidi ya yote tuwe waaminifu kwa nchi yetu,”
alisema.
“Ni aibu kukuta Mtanzania anaitukana nchi yake. Tupende vijiji vyetu,
tarafa zetu, mikoa yetu na nchi yetu. Tuipende, tuitunze na tuilinde ili iwe
nchi bora. Tuwe mfano kwa watoto wetu na wazazi wetu katika kuijali nchi yetu,”
alisisitiza.
Naye, Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Kabudi alipopewa nafasi awasalimie
wananchi, alisema kuna watu wanakufa lakini bado wanaendelea kuwa hai na
kwa hilo, wanafamilia wanapaswa kuendelea kumshukuru Mungu.
"Tangu alipofariki mwaka 1984, hakuna mtu aliyejua kwamba hadi
sasa, ambapo ni miaka 34 imepita, Edward Moringe Sokoine ataendelea kuwa hai.
Ninasema yu hai kwa sababu maneno na matendo yake, bado yanaishi,” alisema.
“Edward Moringe Sokoine amegoma kufa na Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere
amekataa kufa. Na sisi wasaidizi wa Rais Magufuli, tunapaswa kujitoa kwa
wananchi na Taifa; kujiongeza zaidi katika utumishi wetu na hasa kuwajibika kwa
kulitumikia zaidi Taifa kuliko kudai mapato ili tutakapoitwa kwenye promosheni
iliyo kuu, wanaosalia waone faida ya kuwepo kwetu hapa duniani,” alisema huku
akishangiliwa.
Akitoa shukrani kwa niaba ya familia, msemaji wa familia ya marehemu
Sokoine, Bw, Lembris Kivuyo alisema wanaishukuru Serikali kwa jinsi ambavyo
imekuwa karibu sana na familia hiyo tangu Mhe. Sokoine alipofariki.
“Tunaishukuru sana Serikali na tunazidi kuwasihi Watanzania waendelee
kumuombea Mheshimiwa Rais Magufuli ili aendelee kuongoza Taifa hili bila ajizi
na sisi kama familia tutaendelea kumuunga mkono Mhe. Rais katika jitihada zake
za kutetea rasilmali za Taifa,” alisema.
No comments:
Post a Comment