Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa amezungumzia juu ya umuhimu wa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB), kutangaza huduma wanazotoa za ujenzi ili kuwawezesha wananchi kuelewa na kuzitumia huduma hizo na hivyo kuboresha Sekta ya Ujenzi hapa nchini.
Akifungua semina ya siku mbili ya maadhimisho ya ishirini na tisa ya elimu endelevu kwa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi jijini Dodoma Mei 18,2018 Waziri Mkuu amewataka wataalam hao kujiendeleza kitaaluma ili watoe huduma bora zaidi zinazouwiana na mabadiliko ya sayansi na teknolojia.
‘Ongezeni wigo wa huduma zenu ndani na nje ya nchi ili huduma za ujenzi bora wa makazi katika miji na majini ziwe endelevu na zenye gharama stahiki”, amesema Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.
Waziri Mkuu ameisisitiza bodi ya AQRB kuhamasisha wanafunzi kusoma masomo ya sayansi na mafunzo ya ujenzi ili kuongeza idadi ya wanataaluma wanaoweza kujiajiri na kuajiri watu wengine.
Aidha, amehimiza Wizara ya Ujenzi kushirikiana na Wizara ya Afya na Tamisemi katika ujenzi wa vituo vya afya vya kisasa katika mikoa na halmashauri mbalimbali nchini.
Naye Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, amewataka AQRB kuhakikisha wataalam wake wanashiriki kikamilifu katika miradi mikubwa ya ujenzi inayotekelezwa nchini ikiwemo ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), bandari na barabara ili kuwajengea uwezo mkubwa katika taaluma yao.
Amesisitiza kwamba Wizara imeanza kuandaa viwango maalum vya ujenzi vitakavyotumika katika ujenzi hapa nchini ili kuhakikisha kunakuwa na ustawi katika sekta ya ujenzi na makazi nchini.
Amezungumzia umuhimu wa AQRB kupambana na rushwa, kupunguza ada za ushauri ili kuwezesha wananchi wa kawaida kutumia huduma za kitaalam kutoka kwa wataalam hao.
Bodi ya Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi (AQRB) iliyoko chini ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano inajukumu la kuratibu na kusimamia ujenzi kwa kusajili wataalam na makampuni ya ujenzi, kukagua miradi ya ujenzi na kutoa mafunzo kwa vitendo kwa watalaam wa ujenzi hapa nchini ambapo zaidi ya Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi 1520 wamesajiliwa.
Muonekano wa mabanda mbalimbali ya semina ya siku mbili ya ishirini na tisa ya elimu endelevu kwa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi jijini Dodoma Mei 18,2018
Muonekano wa mabanda mbalimbali ya semina ya siku mbili ya ishirini na tisa ya elimu endelevu kwa Wasanifu Majengo na Wakadiriaji Majenzi jijini Dodoma Mei 18,2018
No comments:
Post a Comment