Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Tanzania nchini
Canada, Balozi Alphayo Kidata ambaye alikwenda kwenye Makazi ya Waziri
Mkuu Oysterbay jijini Dar es salaam kuaga, Mei 23, 2018.
(Picha na
Ofisi ya Waziri Mkuu)
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Tanzania bado inahitaji wawekezaji na
kupitia kwenye uwekezaji, inapata fursa ya mitaji na teknolojia za kisasa.
Ametoa kauli hiyo (Jumatano, Mei 23, 2018) wakati akizungumza na
Balozi wa Tanzania nchini Canada, Bw. Alfayo Kidata ambaye alifika kumuaga
kwenye makazi yake jijini Dar es Salaam.
Waziri Mkuu amemtaka Balozi Kidata atumie fursa ya uwepo wake nchini
Canada kuangalia namna ya kuisadia nchi kuimarisha sekta za kilimo, madini na
utalii.
“Tukiimarisha sekta hizi, uchumi ndani ya nchi unakua lakini pia
tunategemea kutumia nchi rafiki kukuza uchumi wetu wa ndani kwa maana ya kukuza
mitaji na kupata teknolojia za kisasa,” amesema.
“Ukienda huko mkakati wako mkubwa uwe ni kuzingatia mpango wa Taifa wa
maendeleo wa miaka mitano lakini zaidi mkakati wetu wa kukuza uchumi wa viwanda,”
amesisitiza.
Amemtaka Balozi huyo akasimamie pia suala la upatikanaji wa masoko kwa
ajili ya mazao yanayozalishwa nchini ili wafanyabiashara na wakulima wa
Tanzania waweze kuuza bidhaa zao nje ya nchi.
“Hapa nyumbani tuna mazao matano ambayo tumeazimia kuyafufua lakini
masoko ya ndani hayatoshi, kwa hiyo kazi yako mojawapo ukiwa huko ni kututafutia
masoko,” amesema.
Waziri Mkuu amemweleza Balozi Kidata azingatie pia suala zima la kuongeza
idadi ya watalii. “Tunataka ukasaidie kutangaza nchi yetu ili watalii waje
kuona vivutio vyetu. Tunataka kuongeza idadi ya watalii kutoka milioni mbili ya
sasa hadi kufikia milioni tano ifikapo mwaka 2020,” amesema.
Alimtaka Balozi huyo akafuatiilie pia fursa za masomo kwa ajili ya Watanzania
wanaotaka kusoma Canada na Cuba. “Nilipoongea na Makamu wa Rais wa Cuba, aliahidi
kuongeza idadi ya Watanzania wanaotaka kusomea udaktari. Kwa hiyo, ukifika
itabidi ufuatilie ahadi hiyo,” ameongeza.
Waziri Mkuu pia alimsisitizia Balozi Kidata akifika huko awatambue na
kuwaunganisha Watanzania waishio Canada na awahamasishe wafanye kazi ili waweze
kuwekeza nyumbani.
Kwa upande wake,
akizungumza baada ya kuagana na Waziri Mkuu,
Balozi Kidata alisema atahakikisha anayafanyia kazi maelekezo
yote aliyopewa na Waziri Mkuu.
Alisema anatambua kwamba Canada ina idadi ya watu zaidi ya milioni 40 na
atafanya juhudi zaidi za kuitangaza Tanzania ili waje kuona vivutio vilivyopo
nchini. Pia atafuatilia fursa za mafunzo kwa wanafunzi wa Kitanzania.
“Kwenye suala la uchumi wa viwanda, tunahitaji kuwa na uzalishaji wa mazao
ya kutosha. Kwa hiyo tunahitaji kuwana kilimo cha uhakika na cha muda wote
kuliko. Tunahitaji kupata utaalamu na mitaji kwa ajili ya mashamba ya umwagiliaji,”
alisema.
Alisema kuwepo kwa kilimo cha umwagiliaji, kutasaidia kuwe na uhakika wa
upatikanaji wa malighafi zitazakotumika kwenye viwanda.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI
MKUU,
JUMATANO, MEI 23,
2018.
No comments:
Post a Comment