NA TIGANYA VINCENT
RS TABORA
SERIKALI Mkoani Tabora imepiga marufuku uegeshaji wa malori katika maeneo yasiyo rasmi mjini Igunga kwa sababu yamekuwa yakivunja Sheria ya Mipango Miji Namba 8 ya mwaka 2007 na pia yamekuwa yakichangia uuaji miti iliyopandwa kando kando ya barabara kuu.
Kauli hiyo ilitolewa jana mjini Igunga na Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri baada ya kuzindua wiki moja ya upandaji miti kando kando ya barabara kuu iliyokuwa ikifanywa na wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari katika Wilaya ya Igunga na wilaya nyingine mkoani kote.
Alisema kuwa uegeshaji huo umekuwa ukiisababishia hasara Halmashauri hiyo kutokana na malengo yake ya kupanda miti kukatizwa kwa kwa sababu ya kufa kufuatia kukayangwa na magari yanayoegeshwa katika sehemu hizo zisizo rasmi.
Mwanri alisema kuwa lori litakalokamatwa limeegeshwa na Dereva wake katika sehemu ambayo haikutengwa na Halmashauri ya Igunga, mhusika atatozwa faini ndipo aruhusiwe kuendelea na safari yake mara baada ya mapumziko.
Alitoa wito kwa madereva wa malori kuwa ni vema wakaheshimu Sheria na taratibu zilizopo zinazowataka kuegesha magari yao katika maeneo yaliyotengwa na Halmashauri zote ambazo ziko njia kuu ili kuepusha uharibifu wa miti inayopandwa.
Mwanri alisema kuwa Sheria ya Miapango miji inatoa muongozo ya kupanga mji na sio kufanya shughuli zao na kukaa kiholela holea , hata katika maeneo hawakupangiwa kuaa.
Alisema kuwa Dereva akitaka kupumzika ni vema akapeleka gari kwanza katika eneo lilitengwa kwa ajili ya shughuli hiyo ndipo aende mapumziko na sio kuliacha kando kando ya barabara na kunyaga miti ambayo jamii na Halmashauri imetumia muda na fedha kuipanda.
“Hapa ni mjini ni lazima madereva waheshimu Sheria ya Mipango miji kwa kuegesha magari yao katika maeneo waliotengewa wakati wanapojisikia uchovu na wanahitaji kupumzika…la sivyo tutawakamata na kutoaza faini, sio kila eneo ni la kulaza gari” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.
Alisema kuwa njia kuu ndio uso wa sehemu husika, kwa hiyo kitendo cha kuacha magari yanakaa na kuegeshwa ovyo ovyo barabarani hasa katika sehemu ya Igunga kunaharibifu sura ya Tabora.
Aidha Mwanri alisema kuwa atamchukulia hatua kali Kiongozi yoyote atakayebainika kuendesha vitendo vya kuwafanya madereva walaze malolri katika maeneo yasiyo rasmi kwa maslahi binafsi.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Igunga Revocatus Kuuli alisema kuwa msimamo wao ni kuwa magari yote yanatakiwa yaegeshwe katika eneo maalumu lililotengwa mjini hapo kwa ajili ya kulaza magari, kinyume cha hapo ni kufanya kosa.
Alisema kuwa Dereva atakayekamatwa akiwa amelaza gari lake kando kando ya barabara atachukuliwa hatua yeye na mlinzi wa kulinda gari lake kwa kuwa tayari walishatoa maelekezo.
Aidha Mkurugenzi huyo Mtendaji alitoa wito kwa vijana au watu wanajifanya walinzi wa magari makubwa yanayoegeshwa katika sehemu isiyo rasmi kuacha tabia hiyo na kama wanahitaji fedha waende katika Ofisi za Halmashauri iwapatie kazi za kufanya au maeneo ya kufanyia kazi ili wasivunje Sheria.
Sheria ya Mipango Miji, namba 8 ya mwaka 2007 inaongoza ukuaji wa miji na mpangilio wa ukaaji katika mji husika ikiwemo utengaji wa maeneo kwa ajili ya huduma za jamii, biashara , usafari , afya na mambo mengine yanayoufanya mji uonekano nadhifu.
No comments:
Post a Comment