Na Dotto Mwaibale, Singida
SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) Mkoa wa Singida wameadhimisha wiki ya huduma kwa wateja kwa kukutana na wateja wao ili kujua changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.
Akizungumza jana katika maadhimisho hayo Meneja wa Tanesco Mkoa wa Singida Mhandisi Florence Mwakasege alisema pia walitumia maadhimisho hayo kuwafikia wateja maeneo mbalimbali kwa ajili ya kuwajulisha huduma wanazotoa.
Alitaja maeneo hayo kuwa ni kwenye masoko, mikusanyiko ya watu na kuwatembelea baadhi ya wateja wakubwa na kuwapa zawadi mbalimbali kwa ajili ya kuwashuku kutokana na ushirikiano wanaoutoa kwa shirika hilo.
Alisema mbali na matukio hayo waliandaa keki maalumu walioila pamoja na wateja wao ikiwa ni ishara ya kuwathamini na kuonesha mahusiano mema baina yao.
Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa Shirika hilo Mkoa wa Singida, Rehema Mwaipopo alisema lengo la wiki ya maadhimisho hayo ni kuwashukuru wateja kwa mchango wanaowapa katika kufanya shughuli zao na huduma wanazo wapa kwa ujumla.
“Kama mnavyofahama bila ya kuwepo wateja hata uwepo wetu sisi wafanyakazi unakuwa katika eneo hatarishi, wateja kwetu ni msingi ndio maana tumekuwa na hii wiki ya kuwashukuru” alisema Mwaipopo.
Alisema Tanesco katika wiki hiyo kuna vitu vingi wamevifanya katika kuboresha huduma zao lakini viwili kati ya hivyo ni mifumo waliyoianzisha kwa ajili ya kurahisisha huduma kwa weteja.
Alitaja mfumo wa kwanza kuwa ni wa NIKONEKT na wa pili ni wa Nihudumie na kuwa mfumo huo wa kwanza unawawezesha wateja kuomba maombi ya kuunganishiwa umeme bila ya kufika ofisi za Tanesco bali muombaji anakuwa nyumbani kwake na atatumia simu janja kuomba maombi hayo wataunganishiwa umeme ndani ya siku nne au saba.
Akizungumzia mfumo wa pili wa Nihudumie alisema ni mfumo wanaotumia namba moja kwa huduma kwa wateja ambayo ni 07485500000 ambayo inatumika na wateja wao mkoa mzima na itatumika nchi nzima siku za mbeleni na kwa sasa inatumika kanda tatu.
Alisema mfumo huo umepunguza changamoto walizokuwa wakizipata wateja wao wakieleza kuwa simu hazipokelewi zimepunguwa na kuwa sasa wameanzisha vituo vidogo vidogo wanavyo viita Viunga kwa ajili ya kuwafikia wateja wao kwa haraka.
Alisema kwa mfumo huo ndani ya nusu saa au masaa mawili mteja wao anakuwa amefikiwa na kupatiwa huduma jambo hilo limeipunguzia shirika hilo malalamiko yaliyokuwepo hapo awali na kuwa wanafurahia huduma hizo.
No comments:
Post a Comment