Mtaalam wa Maabara Kitengo cha Damu Salama Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida, Herjinder Jaswant Hunjan akizungumza na wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha tatu wa Shule za Sekondari Lulumba,,Iguguno, Mwanamwema Shein, Mwanzi na Ikungi katika kongamano la Malezi na Makuzi lililoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Singida kupitia idara ya vijana lililofanyika mwishoni mwa wiki Ukumbi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) Kampasi ya Singida.
Mratibu wa programu ya malezi na makuzi kwa vijana ambaye pia ni Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani akizungumza katika kongamano hilo.
Mgeni rasmi katika kongamano hilo Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Sophia Kizigo akizungumza.Mtaalam wa Maabara Kitengo cha Damu Salama Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida, Herjinder Jaswant Hunjan akizungumza na wanafunzi hao kuhusumakundi ya damu.
...................................
Dotto Mwaibale na Philemon Mazalla, Singida
IMEELEZWA kwamba mimba za utotoni si salama kwa
wasichana wadogo kwani zinachangamoto zake siku za usoni pale msichana husika
anapohitaji kupata watoto baada ya kuwa
kwenye ndoa.
Hayo yamebainishwa na Mtaalam wa Maabara Kitengo cha Damu Salama wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Singida, Herjinder Jaswant Hunjan wakati akizungumza na wanafunzi wa kidato cha kwanza na cha tatu wa Shule za Sekondari za Lulumba,Iguguno,Mwanamwema Shein,Mwanzi na Ikungi katika kongamano la malezi na makuzi ndani ya mfumo rasmi lililoandaliwa na ofisi ya mkuu wa mkoa wa Singida kupitia idara ya vijana.
Hunjan alisema mimba hizo si salama kabisa lakini
kutokana na kukua kwa teknolojia baadhi ya wanafunzi kwa kuogopa kuitwa
washamba wamekuwa wakizitoa kwa kutumia njia mbalimbali lakini balaa linaibuka
baadae baada ya kupata mume mwema na kuhitaji kupata watoto kwani kila mimba
itakapoingia inakuwa inatoka na ndipo kila sababu zinapoanza kutokea mara mama
mkwe au wifi zangu wananionea wivu kwa kuwa sipati mtoto na maneno mengine
mengi yanayofanana na hayo kumbe sababu inakuwa ni msichana husika.
"Hapo hakuna mchawi zaidi ya msichana husika
kwani wakati unazibeba mimba hizo hukuzingatia upo kwenye kundi gani la damu
inawezekana upo katika kundi tofauti na la mume wako hivyo ulipokuwa ukizibeba
na kuzitoa ulikuwa ukitengeneza sumu ambazo sasa zimekuwa kisababishi kikubwa
cha kuharibu mimba ambazo unapata" alisema Hunjan.
Hunjan aliwasisitiza wanafunzi hao kuacha kufanya
vitendo hivyo badala yake wasubiri wamalize masomo na kubeba mimba wakati
watakapokuwa wanazihitaji baada ya kupatiwa ushauri na wataalam na si
vinginevyo kwani njia hizo za kuzitoa zinaathari kubwa.
Mratibu wa programu ya malezi na makuzi kwa
vijana ambaye pia ni Afisa Vijana Mkoa wa Singida, Frederick Ndahani
alisema programu hiyo wameianzisha
mkoani hapa kwa malengo ya kuwajenga wanafunzi wa shule za msingi na sekondari
ili waweze kujitambua katika masuala mbalimbali yakiwemo ya afya na afya ya
uzazi kwa ujumla.
Alisema lengo lingine la programu hiyo ni kuwapa
elimu ya malezi na maadili hasa katika kipindi hiki cha utandawazi vijana wengi
wamekuwa hawana nidhamu na maadili ndio maana wakaona wafanye kongamano hilo
ili kuwajengea uwezo watoto hao kuanzia ngazi ya chini.
"Jambo lingine tunalowafundisha wanafunzi
hawa ni umuhimu wa kuwa wazalendo wa taifa letu kwa kukataa rushwa,
kujitolea kufanya kazi za maendeleo, kukemea pale watakapoona kuna jambo la
kihalifu likifanyika na mambo mengine yanayofanana na hayo" alisema
Ndahani.
Alisema wanafunzi katika kongamano hilo waliimba wimbo wenye maudhui ya kauli mbiu isemayo Mwili wangu Maisha yangu katika ulimwengu wa Kidigitali, waliulizwa maswali ya ujumla ya kupima ufahamu kwa kutaja mikoa ya Tanzania kupitia Ramani ambapo pia walionesha maonesho ya shughuli za mikono na ubunifu.
Pia walipata mafunzo kuhusu afya ya uzazi kwa vijana na jinsi ya kujikinga na UKIMWI/VVU na mgonjwa ya zinaa, elimu ya damu, kuzuia na kupambana na Rushwa, Maadili, Nidhamu na uzalendo na Stadi za Maisha.
Katika kongamano hilo mshindi wa jumla ilikuwa ni Shule ya Sekondari Mwanzi na wa pili Lulumba na kuwa lengo kuu la Programu ya Malezi na Makuzi ni kuwajenga Vijana kutambua thamani ya Mwili wao na namna ya kuutunza ili kufikia malengo kwa kupata elimu ya masuala mbalimbali ikiwemo Haki,Afya na Lishe, uzalendo na uwajibikaji.
No comments:
Post a Comment