Na Dotto Mwaibale, Singida.
KATIBU Tawala Mkoa wa Singida, Dorothy Mwaluko amewapongeza Maafisa Afya
mkoani hapa kwa kazi nzuri wanayoifanya ya kutekeleza kampeni ya Taifa ya Usafi
wa Mazingira katika maeneo yao.
Mwaluko,ametoa pongezi hizo leo Septemba 16, 2022 wakati wa kikao kazi cha
Maafisa Afya kutoka halmashauri za mkoa wa Singida katika hotuba iliyosomwa kwa
niaba yake na Mganga Mkuu wa Mkoa wa
Singida Dk.Victorina Ludovick.
Mnafanya kazi nzuri ya kutekeleza kampeni ya Taifa ya Usafi wa Mazingira
lakini lazima mhakikishe fedha
inayotolewa na serikali matokeo yake yanaonekana na si vinginevyo” alisema
Mwaluko.
Aliongeza kuwa Wakurugenzi wa Halmashauri,Waganga Wakuu, Maafisa Afya na
Watendaji wa vijiji na kata wasimamie ili kuhakikisha kila kaya inakuwa na choo
bora.
Alisema taarifa zilizopo hadi 31 Julai, 2022 kaya zenye vyoo katika Mkoa wa
Singida ni asilimia 99.2 na zisizokuwa na vyoo ni asilimia 0.8, zenye vyoo bora
ni asilimia 62.1 kutoka asilimia 27.6 mwaka 2015.
"Mimi kama Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida, sitavumilia kuona
magonjwa ya aibu kama vile kipindupindu yakitokea katika mkoa wangu hivyo
mjipange katika hili," alisema.
Aidha, alisema Maafisa Afya watambue kuwa wao kama wasimamizi na
wafuatiliaji Wakuu wa shughuli za chanjo, ukaguzi wa dawa, ukaguzi wa vyakula
na ukaguzi wa vituo vya kutolea huduma za Afya mashuleni na taasisi zote
waongeze bidii kusimamia hayo.
Alisema serikali ya awamu ya sita inathamini sana suala la usafi wa
mazingira kwani ndio mhimili mkubwa wa Afya ya Watanzania na ukuaji wa uchumi.
"Tumieni sheria ya Afya ya Jamii ya mwaka 2009 na kanuni Zake,sheria
ya usimamizi wa mazingira ya mwaka 2004 pamoja na sheria ndogo za miji
kuhakikisha maeneo ndani ya Mkoa wa Singida hayachafuliwi hovyo ikiwemo
barabara kuu,stendi,masoko,mitaro,maeneo ya wazi,makazi na makaburi,"
alisema.
Mwaluko alisema maeneo ya masoko na biashara wananchi waweke vyombo vya
kuhifadhia taka vyenye ukubwa wa kutosha kulingana na uzalishaji wa taka kwa
lengo la kupunguza taka kuzagaa ovyo mitaani.
"Kuna maeneo ambayo tumeona hadi yanarushwa kwenye mitandao, Manispaa
(Singida) ndio kioo chetu cha Mkoa wa Singida tuhakikishe usafi unafanyika
maeneo yawe safi," alisema.
Alisema yapo baadhi ya magari ya abiria yanasimama maporini na abiria
kuchimba dawa (kujisaidia) vichakani jambo ambalo halikubariki hivyo Maafisa
Afya wahakikishe wanachukua hatua.
Afisa Afya Mkoa wa Singida, Mgeta Sebastian, alisema maeneo mengi ya mijinj
hata yale ambayo wanapita viongozi wakuu ni machafu sana na kwamba wakati sasa
umefika kwa Maafisa Afya kuhakikisha wanasimamia ili kuweka mazingira safi.
Sebastian alisema katika suala la usimamizi wa afya atakuwa mkali na kwamba
afisa afya asiyetekeleza majukumu yake kama inavyotakiwa atachukuliwa hatua
ikiwamo kumripo kwa wakuu wake.
Aidha Sebastan aliwataka maafisa hao kujenga tabia ya kutoa taarifa za mara
kwa mara za utendaji kazi wao jambo litakalosaidia ufanisi wa kazi na hakuna
sababu ya kusukumana katika jambo hilo.
No comments:
Post a Comment