About Me

header ads

SKAUTI YAJIPANGA KUWAANDAA VIJANA KUTOA MISAADA WAKATI WA MVUA ZA ELNINO

Kamishna Mkuu wa Chama Cha Skauti Tanzania (TSA), LT Abubakar Mtitu  akihutubia wakati akifungua Warsha ya Skauti na wadau wa utoaji huduma za kibinadamu, iliyofanyika Septemba 9,2026 Jijini Dodoma. 

.................................................

Na Mwandishi Wetu, Dodoma.

KAMISHNA Mkuu wa Chama Cha Skauti Tanzania (TSA), LT Abubakar Mtitu amesema chama hicho  kimejipanga vyema na kuwaanda kikamilifu vijana wa Skauti kuchukua hatua za tahadhari kwa kutoa msaada ya kibinadamu kabla na baada ya majanga ya Mvua za El Nino zinazotarajiwa kunyesha katika kipindi cha Mwezi Octoba na Desemba mwaka huu.

LT Mtitu amebainisha hayo leo Septemba 9, 2026 wakati akifungua warsha ya wadau wa chama cha Skauti chenye lengo la kujadili masuala ya utoaji wa misaada ya kibinadamu na usimamizi wa maafa.

Alisema pamoja na mambo mengine chama kinahitaji vijana wa Skauti kuwa sehemu ya mnyororo huo wa Tahadhari ya mapema na hatua za mapemaa, kwa kusaidia kufikisha taarifa, kuhamasisha jamii na kujenga uwezo wa vijana wa kukabiliana na dharura.

"Tunawaomba wadau wetu siyo tu mtupe ushauri, bali pia mtushirikishe, mtusaidie kujenga uwezo na mtengeneze fursa za vijana wa Skauti kushiriki zaidi katika shughuli za maendeleo na huduma kwa jamii" alisema LT Mtitu 

Akizungumza mara baada ya kuwasilisha mada juu ya mwelekeo wa hali ya hewa na El Niño, Mtaalam wa Hali ya hewa na mabadiliko ya Tabia nchi kutoka Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), Daniel Masunga alisema kwa sasa Hali ya El Nino inazidi kuongezeka kadri siku zinavyoendelea  na kwamba Tanzania ipo kwenye zaidi ya nyuzi joto 2 mpaka sasa kwa hiyo inatarajiwa kuwepo na El nino yenye nguvu kubwa.

Amebainisha kuwa maeneo yatakayoathirika  zaidi ni yale yanayopata mvua mara mbili kwa mwaka ikiwemo mikoa ya Kanda ya Ziwa, Nyanda za Juu Kaskazini Mashariki na ya Kanda ya Pwani kuanzia Oktoba hadi Disemba na kuanzia Mwezi Machi hadi Julai.

"Nimefurahi kutoa wasilisho hili katika Chama cha Skauti Tanzania kwa sababu nimejifunza kwamba hawa ni wadau muhimu sana wa usambazaji wa taarifa za hali ya hewa kwa sababu wanamakundi makubwa ya vijana kuanzia shule za msingi, sekondari na hata vyuoni," alisema Masunga.

Naye Afisa Oparesheni wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Dodoma, ASF Stephen Katte amesema pamoja na kwamba jeshi hilo ndiyo linawajibu wa kwanza katika masuala ya majanga bado linahitaji ushirikiano mkubwa kutoka kwa wadau ikiwemo chama hicho cha Skauti Tanzania.

"Warsha hii imetujenga na kutuweka pamoja,  endapo kama janga likitokea basi tunakuwa na ushiriki wa asilimia 100 kwa lengo la kusaidia mwananchi aliyepata matatizo katika majanga mbalimbali ndiyo maana ya kuwepo kwa taarifa kutoka TMA juu ya uwepo wa El nino wadau wote tumeungana" amesema ASF Katte.

  Kamishna Mkuu Msaidizi, Maafa na Ubinadamu, LT Mary Anyitike ameeelza kuwa mara baada ya kupata Elimu ya El nino kutoka kwa wadau,  kazi kubwa iliyobaki ni kwa Skauti kuhakikisha Elimu hiyo inashuka chini katika jamii inayowazunguka ili kuhakikisha Tanzania inavuka salama kwenye janga hilo.

" Vijana wetu wapo tayari kikubwa tunachokifanya kwanza ni kubainisha maeneo hatarishi pindi janga litakapo tokea ili pale itakapo hitajika missada ya kibinadamu tuweze kuwafikia na kutoa huduma kwa nafasi yetu" amesema LT Anyitike.

Mtaalam wa hali ya hewa, Daniel Masunga, akitoa mada kwa wadau juu ya mwelekeo wa mvua za elinino kwenye warsha hiyo. Mhandisi Marwa Magoti kutoka Wizara ya Uchukuzi akichangia mada kwenye warsha hiyo

 Mdau akichangia jambo kwenye warsha hiyo.

Habari hii imehaririwa na Dotto Mwaibaaale Simu namba 0754362990

Post a Comment

0 Comments