WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii irudi kwenye maeneo yote yenye migogoro ya mipaka na iungane na Halmashauri za wilaya ili waweze kutoa majibu kwa wananchi.
Waziri Mkuu ametoa agizo hilo (Alhamisi, Februari 8, 2018) wakati akijibu swali la mbunge wa Urambo, Bibi Margaret Sitta wakati wa kipindi cha maswali ya papo kwa papo kwa Waziri Mkuu Bungeni mjini Dodoma.
Bibi Sitta alitaka kujua Serikali imeweka taratibu na mikakati gani ya kumaliza migogoro ya mipaka inayoendelea katika maeneo mbalimbali ya hifadhi za misitu nchini kwa kuwa wananchi wanahitaji maeneo kwa ajili ya shughuli za kilimo na mifugo.
Waziri Mkuu amesema Serikali iliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii iweke vigingi kwenye maeneo yote yanayozunguka hifadhi za misitu ili kuweka alama zitakazopunguza migogoro ya kuingiliana kati ya wananchi walioko kwenye vijiji na wahifadhi kwenye maeneo ya hifadhi ya misitu hiyo.
Amesema maagizo hayo yalitolewa baada ya kugundua kuwa kuna migogoro mingi kati ya wananchi walioko katika vijiji vya jirani na misitu iliyohifadhiwa kisheria ambayo ina ramani.
“Lakini tunatambua kwamba wanapoendelea na zoezi hilo la uwekaji alama, inaweza kutokea kijiji kikajikuta kipo ndani ya mipaka ya hifadhi na inaweza kusababisha kutoelewana kati ya wanakijiji na wenye mamlaka ya hifadhi.”
“Tuliwasihi wanakijiji wakati zoezi hili linaendelea na hata kama kijiji kitajikuta kimezungukwa na hizo alama, wanakijiji watulie ili kazi ya awali ikamilike na pale kwenye mgogoro, Serikali itarudi tena kuja kuangalia mgogoro huo na kufanya tathmini ya kina.”
Amesema Serikali iliiagiza Wizara ya Maliasili na Utalii inapofanya kazi hiyo ya kuweka vigingi lazima ishirikishe mamlaka za halmashauri na kijiji husika na wao washiriki katika zoezi hilo ili kuondoa migogoro isiyokuwa ya lazima.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali ilishaielekeza Wizara ya Mifugo na Uvuvi izitumie ranchi za NARCO na kugawa katika vitalu ili kubaini ukubwa wa eneo iliyonayo ndipo iweze kufanya uamuzi wa kugawa vitalu hivyo kwa wafugaji.
Ameyasema hayo wakati akijibu swali la Mbunge wa jimbo la Nkenge, Balozi Dkt. Diodorus Kamala aliyetaka kujua taarifa ya kamati iliyoundwa na Serikali kufuatilia migogoro ya ranchi zilizokuwa chini ya NARCO na wafugaji, itapelekwa lini bungeni ili iweze kujadiliwa.
Waziri Mkuu amesema Wizara ya Mifugo na Uvuvi iliunda tume ya kufuatilia maeneo yote ya ranchi za Taifa na kuyapima maeneo hayo lakini pia kujua ni akina nani wanayamiliki maeneo hayo, kubaini kama walipewa kihalali, na kama ni kweli wanamiliki mifugo yoyote kwenye maeneo tajwa.
Kuhusu kupelekwa bungeni kwa taarifa ya tume hiyo, Waziri Mkuu amemtaka Waziri wa Mifugo aikamilishe na kuiwasilisha Bungeni kama taratibu zinavyotaka ili kuwawezesha wabunge na wananchi wajue dira na mwelekeo wa Serikali wa namna ya kufuga mifugo hiyo kwa njia ambazo zitawaletea tija lakini kikubwa zaidi ni kumaliza migogoro baina ya wakulima na wafugaji.
No comments:
Post a Comment