Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa Kigoma Michael Maganga akitoa taarifa kuhusu ajali ya majini iliyosababisha vifo vya watumishi sita wa Halmashauri ya Wilaya ya Kigoma Machi 13, 2026.
...........................
Na Mwandishi wetu, Kigoma
Watumishi sita wa Halmashauri ya wilaya Kigoma mkoani Kigoma wamefariki dunia kati ya watumishi 18 waliokuwa wakisafiri kutoka Kigoma Mjini kuelekea kijiji cha Kagunga halmashauri ya wilaya Kigoma kwa shughuli ya kutoa chanjo baada ya boti yao kukumbwa na upepo ziwa Tanganyika na kupinduka.
Mkuu wa jeshi la Zimamoto na uokoaji mkoa Kigoma, Michael Maganga akizungumza na waandishi wa habari eneo la tukio amesema kuwa tukio hilo lilitokea majira ya saa mbili asubuhi Machi 13 mwaka huu katika kijiji cha Kalalangabo Halmashauri ya wilaya Kigoma ambapo pamoja na hao waliothibitika kufa na miili yao kupatikana pia watu wengine watatu waliokuwa kwenye boti hiyo hadi sasa miili yao haijapatikana.
Maganga amesema kuwa watu wengine tisa ambao pia walikuwa kwenye boti hiyo wameokolewa na kwa sasa wanapatiwa matibabu katika hospitali ya rufaa ya mkoa Kigoma Maweni huku juhudi za kutafuta miili ya watu watatu ambao hawajapatikana ikiendelea.
''upepo mkali ulioanza majira ya asubuhi unaelezwa kuwa chanzo cha ajali hiyo." Amesema.
Akizungumzia ajali hiyo mmoja wa mashuhuda waliosaidia kuokoa watu kwenye boti hiyo ya Halmashauri, Hababu Ibrahim Mwenyekiti wa kitongoji cha ziwani amesema kuwa alipata habari akiwa nyumba majira ya asubuhi ndipo akateremka ziwani na kusaidia zoezi hilo la kuokoa watu waliokuwa kwenye boti hiyo.
Mkuu wa mkoa Kigoma, Balozi Simon Sirro alifika eneo la tukio na kutoa pole kwa uongozi wa Halmashauri ya wilaya Kigoma na familia za watu wote waliopatwa na tukio hilo na kwamba serikali ipo karibu kuangalia mambo yote na kutoa msaada wowote utakaohitajika.


0 Comments